Ndugu msomaj habari za siku ya leo. Nakukaribisha katika makala ya leo.
Ajira kwa sasa ni changamoto kubwa sana hasa hasa kwa vijana na pia katika nchi zinazoendelea hasa dunia ya tatu. Si tu katika kuipata bali pia katika kuifanya.
Labda nianze kwa kukueleza kuwa tangu nikiwa mwanafunzi mpaka sasa nimebahatika kukutana na wafanyakazi wengi ambao wamekuwa wakilalamika kuhusu kazi zao, nazungumzia katika kada nyingi nilizobahatika kukutana nazo hasa wafanyakazi wa ngazi ya chini na kati. Kila mtu analalamika kuhusu kitu ambacho yeye anakikosa anatendewa. Lakini wengi wamekuwa wakilalamika kuhusu maslahi duni (mishahara na marupurupu), mazingira magumu ya kazi, manyanyaso kutoka kwa wakubwa wao wa kazi, kudharaulika, kupuuzwa na hata kutokusikilizwa na mengine yanayofanana na haya.

Mbali na kwamba tatizo linaweza kuwa kwa wanaolalamikiwa kwa kutotekeleza majukumu yao pia kuna wafanyakazi wasiotekeleza majukumu yao. Hilo tatizo pia tatizo kubwa ni kwamba wafanyakazi wengi wamekuwa watu wa kulalamika bila kuchukua hatua. Unakuta mtu kaajiriwa mwanzoni mwa miaka ya tisini bado analalamika kuhusu hali aliyoikuta bila yeye kashindwa kuibadili au yeye mwenyewe kubadillika. Kulalamika na kulaumu kamwe hakuwezi kutatua tatizo lako kazini bali kuchukua hatua pekee ndio njia ambayo inaweza kusaidia. Kuna hatua kadhaa ambazo utatahitaji kuchukua kama mfanyakazi ambaye unaona hautendewi inavyopasa.
Hatua ya kwanza ni kubadili mtazamo kuhusu kazi unayoifanya. Jitathmini na kuweza kugundua wapi kuna tatizo kati yako na mwajiri wako. Yawezekana kuna matatizo kidogi kwenye ajira yako kulinganisha na wewe unavyochukulia. Mapungufu hayawezi kukosekana popote hivyo mengine yapasa uyazoee na kuchukulia kama sehemu ya changamoto za kazi. Matatizo mengi yanaanza kwenye mtazamo wako (attitude) kuhusu jambo fulani. Kama ukijenga mtazamo hasi basi utaona kila kitu ni kibaya lakini ukiojenga mtazamo chanya utaona mazuri kuliko mabaya. Kama pia wewe ni muoga kuchukua hatua ambayo nitaitaja hapa chini basi bora ukubaliane na kazi yako na kuamua kuifanya kwa moyo wako. Wengine ni waoga sana kuchukua hatua hiyo, huwaza wataishije. Jipime na uangalie kama unaweza kubadili kitu kibadili na kama huwezi kubadili kubaliana na hali halisi iliyopo.
Kubadili kazi yako kwa kufanya kazi nyingine. Ndugu yangu hii ni hatua ngumu sana kwa watu walio wengi hasa ambao wamekaa kwenye ajira kwa muda mrefu na pia wana majukumu mengi. Najua ilivyo ngumu sana kuacha kazi ambayo ndiyo ilikuwa kila kitu kwako lakini kama haikupi yale ambayo ulikuwa ukiyapata kabla huna budi kujikaza na kuchukua hatua hii. Mwanafizikia maarufu zaidi wa karne ya 20 aliwahi kusema kwama kuendelea kufanya kitu kile kile kwa namna ile na kutegemea matokeo tofauti ni ujinga. Kwa mfano umekuwa ukilipwa hela ndogo sana kiasi kwamba huwezi hata kujiwekea akiba ama hautoshelezi kiasi kwamba unaweza kuwa unaishi kwa madeni tu na wakati huo ukitegemea kufanikiwa katika kujiletea maendeleo utakuwa ni zaidi ya muujiza. Sisemi kwamba wote wanaoshindwa kujiwekea akiba kunatokana na kulipwa hela ndogo, la hasha kuna wengine wanshindwa kujiwekea akiba kutokana na matumizi yao mabovu ya hela. Ila kuna wengine kweli ni ngumu kujiwekea akiba kwa vipato vyao vidogo na majukumu mengi. Suluhisho hapo ni kutafuta kazi nyingine unayoipenda kabla hujaacha uliyonayo ama kuanza kufanya shughuli nyingine tofauti na ajira yako yaani kujiajiri au ujasiriamali. Pia kuna mtu aliwahi kusema Kama kile unachofanya hakikupi tena faida ni bora kukiacha. Kunahitaji ujasiri mkubwa sana kwa baadhi ya watu kuacha kazi. lakini kabla hujaogopa kuacha kazi, jaribu kujiuliza itakuwaje siku ukifukuzwa kazi? Je utaishije, je utakufa? naomba ujijibu mwenyewe. Tatizo la wafanyakazi wengi ninkwamba hawajiandai kustaafu tokea siku ya kwanza ya ajira. Kumbuka huna uhakika na ajira yako maana huhusiani moja kwa moja na mwajiri wako kiasi kwamba utafanya kazi hiyo mpaka ufikie umri wa kustaafu kwa lazima. Hivyo basi ni muhimu kujipanga kabla hujapangwa. Ni bora kabisa uanze kutafuta vyanzo vingine vya mapato kwa kujiajiri, kufanya biashara au ujasiriamali wakati ukiendelea na kazi unayoifanya ili ikitokea umeacha basi uwe na pa kuanzia.
Soma: Je umepanda nini shambani kwako?
Soma: Je umepanda nini shambani kwako?
Wengine huogopa kuacha kazi kwa sababu hawana akiba yoyote waliyojiwekea. Yaani maisha yake ni kula tu yaani anafanya kazi aishi, waingereza husema Living hand to mouth. Ndugu yangu ukiishi hivyo ujue kwamba hakika utakufa masikini. Sikutabirii ila ndio ukweli wenyewe huo. Mtu mmoja aliwahi kuniambia usiishi kama mvuvi (samahani wavuvi), kwani wavuvi walio wengi hawaamini katika kujiwekea akiba maana anajua ziwa, mto ama bahari wanakovua zipo milele na atavua tu. Tabia hii huwafanya watumie mapato yao vibaya na kushindwa kujisaidia wakati ambapo hawana nguvu, wagonjwa, wamezeeka ama hakuna tena samaki kwa kipindi fulani au serikali kusitisha uvuvi ili kuruhusu samaki kuzaliana.
Nipende kuhitimisha tu kwa kukuambia kuwa kuendelea kulaumu, kunung´unika ama kulalamika hakutasaidia kama wewe hujaamua kutafuta suluhisho. Kumbuka kwamba maisha ni yako na mfanya maamuzi ni wewe. Ukiamua kuendelea kulia ni sawa pia na ukiamua kuchukua hatua ni bora zaidi. Changamoto ni sehemu ya maisha na uchaguzi ni wako uishije, mfano unaweza kuhainga sasa hivi ukaishi vizuri kesho ama uishi kwa starehe leo ukahangaike kesho.
Nyakati ngumu hazidumu lakini watu wagumu hudumu (Tough times never last but tough people do),nimenukuu kutoka kwa mwandishi Robert H.Schuller.
Nakutakia siku njema, kwaheri.
Nickson Yohanes
Email: nmyohanes@gmail.com