Habari za leo ndugu msomaji wa
mtandao huu wa PAMBAZUKA DAIMA ni
matumaini yangu kwamba bado unaendelea kulisukuma gurudumu la maendeleo kwa
kufanya kitu bora zaidi ya ulivyofanya jana.
Ndugu msomaji kuna siri katika
kila kitu ambacho ukifanikiwa kuijua basi utaweza kufanikiwa katika eneo
husika. Kuna siri za kufaulu mitihani shuleni, kuna siri za kuwa na familia
bora na kadhalika. Naita siri lakini kiukweli sio siri kwani ni vitu ambavyo
tunavijua ama tunaona kwamba havina maana katika maisha yetu na hivyo kutotilia
maanani.
Labda nianze kwa kukuuliza swali
hili; Ikiwa una ndoo ya maji iliyojaa maji tayari, ukitaka kuweka kitu kingine
katika ile ndoo au maji mengine utafanyaje? Majibu yanaweza kuwa mengi lakini
jibu la muhimu ni kuyatoa yale maji kwa kumwaga ama kumpa anaehitaji ili upate
nafasi ya kuweka kitu kingine. Lakini litakuwa sio jambo jema kumwaga maji
wakati kuna anaehitaji. Kwa hiyo basi siri ya kupokea kitu chochote ni kutoa,
ndio kutoa kwa anaehitaji ili nawe upate nafasi ya kupokea kitu kipya. Kama
hutatoa na wewe umeshajaza vitu katika sehemu yako ni dhahiri kwamba hakutakuwa
na nafasi ya kupokea kitu kipya. Ndio maana tunashauriwa kutoa ili nasi
tupokee, huwezi kuwa mtu wa kupokea pekee.
Tunapozungumza suala la utoaji
tunamaanisha kitu chochote ambacho kinaweza kuwa msaada kwa mtu mwingine. Suala
la kutoa sio lazima uombwe, ni muhimu zaidi kama ukitoa bila msukumo kutoka nje. Kitabu
cha biblia kinawaasa watu kuwa kutoa ni bora kuliko kupokea na pia utapokea
kadiri nawe unavyotoa, tena maradufu. Unapozungumzia suala la kutoa watu wengi hupeleka akili
zao katika pesa. Kutoa pesa ni muhimu pia, lakini je kama huna pesa huna sifa
ya kutoa? Unaweza kutoa kitu chochote kwa mtu yeyote ilimradi kina msaada
kwake. Unaweza kutoa msaada, kutoa elimu, kusaidia wasiojiweza, kufundisha
wenzako, kutoa muda wako kwa kusaidia wengine ama kuwatembelea wagonjwa, yatima na wale wanaohitaji faraja na hata kutoa sehemu ya mali zako kwa
wengine. Kuna siri kubwa katika utoaji, ni siri ambayo haiwezi kuelezeka
kirahisi ni siri kubwa sana ya kupokea chochote. Ila muhimu sana ni kwamba
unapotoa kitu usitoe ukingoja shukrani au ukitegemea malipo kwani malipo yake
utapata katika muda usioutegemea tena kwa mtu usiyemtegemea. Kuna msemo wa
Kiswahili usemao ‘’Tenda wema nenda zako,
usingoje shukurani’’.
Soma: Je umepanda nini shambani kwako?
Soma: Je umepanda nini shambani kwako?
Ndugu yangu unaesoma hapa nawe
una kitu cha kutoa kwa watu wengine, usiwe mtu wa kupokea pekee bila kutoa.
Kutoa hakukufanyi kufilisika bali kuendelea kuneemeka. Kama kutoa kungekuwa
kunafilisi basi bilionea tajiri namba moja duniani Bill Gates angeshafilisika
kitambo kwa misaada anayotoa duniani
kupitia mfuko wake wa Bill and Melinda Gates unaohusika kutoa
misaada kwa watu masikini kote duniani. Kwa hapa nyumbani Tanzania basi mzee
Reginald Mengi angekuwa ameshafilisika kitambo pia maana toka nilivyoanza kumsikia
anatoa misaada kwa kweli angekuwa ameshaishiwa. Bilionea namba tatu kwa sasa
ambae pia alishakuwa namba moja na mbili katika kipindi cha nyuma Warren Buffet nae ni
mtoaji mzuri na amedhamiria kutoa 99% ya
utajiri wake kama misaada katika maisha yake yote. Hii ni tofauti kabisa na dhana hasi iliyojengekwa kwamba watu matajiri ni wabinafsi na wachoyo, jambo ambalo si kweli. Matajiri hupenda kusaidia hasa wale wanaonyesha nia ya kufanya jambo fulani zuri.
Kama wewe ni mwanafunzi na
unalijua vizuri somo fulani kuliko mtu mwingine yeyote darasani kwako ukiamua
kulifundisha hilo somo kwa wengine, si tu kwamba utakuwa umewasaidia wengine
kufaulu somo linalowapa shida bali pia nawe utaimarika katika hilo somo kwa
kupokea changamoto na kupokea elimu mpya kutoka kwa wengine.Pia itakusaidia kukumbuka kirahisi na kuonekana bingwa wa somo husika. Utafungua
mlango wa wenzako kukusaidia katika masomo mengine ambayo wanayaweza vizuri kuliko wewe. Kinyume
chake ni kwamba hutaona mafanikio mazuri katika masomo yako kama utakuwa mbinafsi. Kila mtu anaweza kutoa
kitu, hata kama ni kidogo kiasi gani. Ndio maana hata katika dini zetu
tunasisitiziwa kutoa zaka katika nyumba za ibada kama shukurani kwa Mungu wetu kwa aliyotujalia kupata.
Inaweza kukuwia vigumu pale
unapoanza lakin utaweza kuzoea tabia hiyo ya utoaji kadiri unavyotoa kila mara. Unaweza kuanza
kidogo kidogo mpaka pale utakapoona kwamba sasa huoni ugumu katika kutoa. Labda
nikupe hadithi ya kweli; Mwaka fulani nikiwa sekondari, tulitoka shule mchana
kama ilivyo ada. Tukitembea watatu njiani kuelekea nyumbani mmoja wetu (si mimi)
alitoa kiasi fulani cha pesa kwa mlemavu aliekuwa anaomba barabarani, hatua kama tano
mbele aliokota mara tano ya pesa aliyotoa kwa yule mlemavu. Unaona katika mfano
huu jinsi kutoa kunavyofungua milango mingine, milango ya kupokea. Sikuambii kwamba ukitoa nawe
utaokota hela kama rafiki yagu,hapana. Toa kwa kuwa umeguswa na ukiamini kwamba
unawasaidia wengine kwa kile ambacho umejaaliwa kuwa nacho. Tahadhari tu kwa
upande wa fedha uweze kutofautisha kati ya kutoa kusaidia na kutapanya pesa
zako ovyo. Unaweza kuanza kwa kutenga asilimia ya mapato yako kwa kusaidia
wengine. Muda wako nao ni wa thamani sana hivyo ni muhimu kuulinda na kutoutoa kwa wale wasiostahili.
Usisahau kupenda ukurasa wetu wa
facebook kwa kubonyeza Pambazuka
Daima Blog na pia kujiunga na orodha yetu ya barua pepe kupata makala kila mara
zitokapo.
Nickson Yohanes
nmyohanes@gmail.com