Habari za muda huu ndugu msomaji
wa mtandao huu wa PAMBAZUKA DAIMA.
Ni matumaini yangu kwamba unaendelea kusonga mbele licha ya changamoto za hapa
na pale unazokutana nazo, changamoto hizo ni magurudumu katika safari yako. Kwa wale waliokuwa wananifuatilia hapo zamani watakumbuka kuwa nilikuwa naandika kupitia blog ya Life Adventures ambayo nimehamishia makala zote huku na kwa wasomaji wapya nitumie fursa hii kuwakaribisha.
Ndugu msomaji katika hii dunia
tumezungukwa na vitu mbalimbali. Tumezungukwa na watu, vitu, mimea na hata
wanyama. Vitu hivi vyote vinaweza kutuathiri kwa namna hasi au namna chanya.
Tunaweza kuathiriwa zaidi na binadamu wenzetu kuliko tunavyoweza kuathiriwa na
vitu vingine. Lakini pia sio kila binadamu anaweza kutuathiri bali wale ambao
tunatumia muda wetu mwingi nao. Hao si wengine bali ni ndugu,jamaa na
marafiki. Ndio, hao ndio watu ambao mara nyingi tunapendezwa nao na hivyo kujikuta kwamba tuko nao muda mwingi sana kiasi cha kuweza kutuathiri. Kuna msemo wa Kiswahili usemao
kwamba unaweza kuchagua marafiki lakini huwezi kuchagua ndugu na majirani. Huu
msemo uko sawa kabisa kwani kama ndugu zako si watu wazuri huwezi kuwakataa
kuwa si ndugu zako, vile vile unaweza kuwa na majirani wabaya sehemu unayoishi sasa ama ukajikuta kwamba kila unapohamia unakutana na watu wa ajabu tu. Sote tuna uwezo mmoja mkubwa wa kuchagua marafiki, ndio marafiki tunaoona
tunaendana nao, marafiki ambao tabia zao zitatujenga kuliko kutubomoa. Labda sisi tuliopo katika kizazi hiki cha teknolojia tuna nafasi kubwa ya kuathiriwa hata na watu tusiowafahamu kuliko vizazi vilivyotutangulia hasa kupitia mitandao ya kijamii kama facebook, whatsapp, telegram, tweeter,instagram nk. Tunaweza kujaza hisia hasi ama chanya kwa haraka zaidi kuliko kipindi chochote kingine katika historia ya dunia hii. Bahati mbaya ni kwamba wengi wamekuwa wakitumia mitandao hii kwa kubomoa zaidi kuliko kujenga. Ni muda sasa wa wewe kutafakari aina ya makundi ya kijamii ama watu waliopo mitandaoni unaowafuatilia. Usikae katika kundi au mtandao wa kijamii usiokujenga,bali kaa sehemu ambayo unaweza kuambukizwa chaji chanya za maisha.
Tabia za watu wengine huathiriwa
zaidi na tabia za marafiki zao au watu anaotumia nao muda wake mwingi. Kama
utakuwa na marfiki walevi bila shaka nawe utakuwa mlevi, ukiwa na marfiki wezi
nawe utakuwa vile vile, ukiwa na marafiki wenye mafanikio nawe pia utakuwa na
mafanikio na hata pia ukiwa na marafiki walalamikaji nawe utakuwa mlalamikaji
vile vile. Unaweza kupingana nami lakini ukweli ni kwamba ndege wafananao huruka pamoja.Mafanikio yetu ni wastani wa watu wa tano tunatumia muda wetu mwingi
na wao. Mbuzi hawezi kukaa na mnyama mwingine muda mrefu kama afanyavyo kwa
mbuzi mwenyewe. Tabia za watu walikuzunguka zinaakisi tabia zako. Kama watu
hawana uhakika na tabia zako basi wataangalia tabia za marafiki zako, hii ni
kwa sababu mtu huvutiwa na tabia za wanaomzunguka. Ndugu, jamaa na marafiki
wana nafasi kubwa sana ya kutuathiri na kutufanya tufanikiwe ama tusifanikiwe
katika kile tunachokifanya. Kama una marafiki wakatishaji tamaa nawe utakuwa
mkatishaji tamaa ama mkata tamaa mwenyewe. Marafiki hasi na walalamikaji
watakufanya kuwa mmoja wao na sio tofauti nao, marafiki waoga huwa na marafiki
waoga ama ambao wataambukizwa tabia hizo za uoga.
Ni muda sasa wa kutathmini aina
ya watu wanaokuzunguka kama ni watu wanaokusaidia kusonga mbele ama kurudi
nyuma. Kama ni kundi la kukupeleka mbele basi unaweza kuendelea nao na kama ni
wa kukurudisha nyuma,acha kutumia muda wako mwingi na wao. Sijasema uwatenge la
hasha ila kupunguza ukaribu nao na utafute marafiki wenye malengo sawa na yako, marafiki chanya na marafiki wenye msaada kwako kwa namna moja au nyingine. Kama ni ndugu najua kabisa huwezi kuwakataa kwamba sio ndugu zako bali cha
kufanya ni kutokaa nao muda mrefu kiasi cha kukuathiri, unaweza kutumia muda mfupi tu kujuliana hali ama kujadili masuala muhimu ya familia pale inapobidi. Tafuta watu werevu kama
wewe au kuliko wewe, ambao unaweza kujifunza kutoka kwao. Kuna mtu aliwahi
kusema kwamba kama katika kundi wewe ndiye mtu mwerevu pekee basi ni muda wa
kuliacha hilo kundi na kutafuta kundi lingine. Hii ni kwa sababu badala yaw
ewe kujifunza kutoka kwao utaweteka na kujisahahu ama kujiona wewe ndio kila kitu na kubweteka na huku pia jamaa hao wakikunyonya badala ya kusaidiana.
Usiogope kuwapoteza marafki ambao wanakuvuta kuelekea nyuma, marafiki waliojaa
mawazo hasi au marafiki wanaokunyonya,siku zote kuwa na watu mtakaofaidishana (win-win situation). Utapata marafiki wengine bora zaidi.
Kumbuka kwamba marafiki na watu
walikuzunguka wana nafasi kubwa ya kuamua kiasi cha mafanikio yako, ni lazima
uchukue hatua mara moja kabla hujachelewa. Tafuta watu chanya, watu wenye
kukusongesha mbele, watu wenye kutia moyo na watu wenye kukusaidia pale
unapohitaji msaada wao au watakapoona unahitaji msaada. Kuna marafiki wanawaza
kukata tamaa muda wote, wegine wanawaza starehe muda mwingi na wengine wanawaza
kuhusu namna ya kufanya makubwa. Ni heri uwe peke yako kuliko kuwa na marafiki hasi. Kubali ukatae ukikaa na kundi lolote
nililotaja utaanza kuzoea (adapt) hali hiyo na kuona ni kawaida. Unadhani watu
wengi wameanza kunywa pombe, kuvuta bangi na sigara, ujambazi na tabia
zinazofanana na hizo kupitia nani kama sio ndugu, jamaa na kwa kiasi kikubwa
sana marafiki? Ni vigumu kukutwa kwenye kundi la majambazi halafu watu
wakaamini kwamba wewe sio jambazi.
Marafiki wawe chachu ya wewe
kusonga mbele na sio kukurudisha nyuma. Watu waliofanikiwa hukaa na watu
waliofanikiwa. Watu wasiofanikiwa hukaa na watu wasiofanikiwa, hawachangamani
kama ilivyo kwa mafuta na maji. Kuna msemo wa KIkemia usemao ‘’Like dissolve like’’ ukiwa na maana
kwamba vitu vinavyofanana huyeyushana kwa vyenyewe mfano maji kwa maji na
mafuta kwa mafuta. Hivyo hata kama hukuwa na tabia fulani utaambukizwa kutoka
kwa marafiki zako. Kulikuwa na jamaa ambae kila mwaka mpya wa masomo ukianza
alipokuwa anasoma alikuwa akiwaambia watu kuwa baadhi ya masomo ni magumu sana
na uanaweza kufeli, ama mwalimu fulani ni mbaya. Unajua kilichotokea? Ni kwamba
maneno yake ya kukatisha tamaa na ya kujirudiarudia yaliwaingia baadhi ya watu
moyoni na kwenye akili na kutengeneza ugumu wa masomo husika ambayo hatima yake
ni kwamba walifeli masomo husika. Ugumu aliouona yeye aliwaambukiza marafiki
zake. Sio tu kwamba aliwaambukiza tabia hiyo bali pia tabia zingine ambazo
pengine zisingefaa kwenye jamii iliyostaarabika. Kila mtu ana rafiki, ndugu au
jamaa ambae amemgusa kwa namna moja ama nyingine iwe hasi au chanya. Kila mtu
anaweza kutoa mfano wa rafiki yake mwenye tabia fulani kama akipewa nafasi. Ni
muda wa kukaa mbali na rafiki mwenye tabia kama nilizotaja kwenye mfano ama
ubaki nae uangamie.
Kama kuna mtu ambae alikuwa
masikini na kushinda maskani ama kijiweni, siku akianza kufanikwa hupata
marafiki wenye mafanikio ama alihama kuwatafuta watu wenye mafanikio wenzake.
Ni vigumu sana kuwakuta matajiri katika vijiwe vya masikini na hii hupelekea
masikini au watu uliokuwa nao kijiweni kusema kwamba umeanza kuringa baada ya
kuanza kutajirika, unakumbuka ‘’like dissolve like?’’. Siku alifanikiwa akianza
kurudi kijiweni kukaa na wale watu wenye mawazo hasi, kuna mawili yanweza
kutokea nayo ni yeye kuwapandisha kwa kuwabadili ( na inaweza kuwa ngumu pia)
ama yeye kurudishwa nyuma ili aweze kufanana nao. Badili marafiki kabla
hajakubadili wewe,badili maisha yako.
Wajali ndugu,jamaa na marafiki
zako kwa kuwatumia makala hii. Pia usisahau kujiunga nasi kwa email ili kupata
makala na vitabu na kuLike page yetu Facebook kwa kunyeza hapa. Kupata makala za Afya,Chakula na Lishe bonye za Hapa
Nickson
Yohanes
nmyohanes@gmail.com