Hbari mpendwa msomaji wa mtandao
huu wa PAMBAZUKA DAIMA ni matumaini
yangu kwamba unazidi kulisongesha gurudumu la kuelekea kwenye mafanikio ya
maisha yako.
Leo ningependa nikushirishe
kuhusu utofauti mmoja uliopo kati ya mfugaji na muwindaji au mvuvi.
Sote tunajua kuwa jamii zote hizi
nilizojata zinategemea wanyama kwaajili ya kuendesha maisha yao, wafugaji wakiwategemea wanyama
wawafuagao huku wavuvi wakitegemea kuendesha maisha yao kwa kuvua samaki na wawindaji wao wakitegemea kuwinda wanyama wa porini kuendesha maisha yao. Japo jamii za uwindaji zinaonekana kama zimekwisha katika
karne hii bado kuna jamii chache sana zinazotegemea kuishi kwa kutegemea
uwindaji.
Mfugaji ni yule mtu anaefanya
kazi ya kuwatunza wanyama na kuwafanya waongezeke maradufu. Huwawekea mazingira
mazuri ya kuishi, matibabu na malisho. Huishi kwa kuwategemea kwa chakula hasa
maziwa na nyama. Muwindaji hachinji wanyama wake ovyo bali huwachinja kwa
utaratibu maalum tena baada ya kuongezeka sana. Umeshawahi kumuona mfugaji
mwenye ng’ombe mmoja akaamua kumchinja? Jibu ni hapana. Kitu kingine ni kwamba
wafugaji wengi huwapenda sana mifugo yao kiasi kwamba hawawachinji au kuwauza
mara kwa mara. Ni kutokana na tabia hii ya wafugaji kujikuta wana mifugo wengi.
Mifugo ninayoizungumza ni ile mifugo ya kawaida ambayo hata Tanzania tunao kama
ng’ombe, mbuzi, kondoo, kuku na hata samaki. Hivyo basi tabia ya mfugaji
tunayoiona hapa ni kusubiri kula mazao yatokanayo na mifugo yake na sio kula
mifugo yake kabla haijazaliana.
Kwa upande wa muwindaji au mvuvi
yeye anaamini kwamba pori, ziwa, mto au bahari zipo tu na samaki wataendelea kuwepo.
Si ajabu kukuta mvuvi au muwindaji kutokuwa na akiba yoyote ya kumtosha kwa
siku kadhaa, si bahari, mto au ziwa lipo bhana?sasa kwanini ahangaike, hamna
sababu (kwa mawazo yake). Tatizo ni pale ambapo atakosa uwezo wa kuvua ama kwa
uzee au ugonjwa, lazima familia itatereka kwa kukosa mahitaji muhimu. Pia kuna
kipindi serikali hufunga mito, mabwawa na maziwa ili kuruhusu samaki kuzaliana.
Wakati huo huo aliefuga samaki anaweza kuendelea kuishi.
Maisha ya muwindaji na mvuvi ni
ya kula na kutumia kile chochote anachokipata, hakuna akiba na wala hakuna
kesho. Mfugaji yeye ana akiba ya mifugo yake na huitumia pale ambapo anapata
tatizo. Muwindaji hawezi kwenda porini kuchukua wanyama walio hai ili
kuwatunza, hana muda wala uvumilivu huo. Muwindaji na mvuvi hawaweki akiba ya
walichokipata ama kukiendeleza ili kiwe kikubwa ili kesho kiwasaidie, hawafikiri katika kuzalisha bali kutumia tu. Hawa watu
wanakula kila kitu na kusahau kukuza ili kesho kiwape faida. Wanasahau kuwa
akiba haiozi.
Mpendwa msomaji mfano wa mfugaji
na mvuvi ni mfano uliopo katika jamii zetu.Inawezekana kabisa wewe una tabia zote za mfugaji au una tabia zote za mvuvi/mwindaji. Ni muda sasa wa kujifanyia tathmini. Kuna wale ambao huweka akiba na
kukuza vipato vyao ili viwasaidie baadae na hao ndio mfano wa mfugaji na kuna wale ambao hutafuna kila kitu
walichojaaliwa kukipata,hawa ndio wavuvi. Bila shaka wewe unajijua upo kundi gani, kundi la
mfugaji au kundi la mvuvi. Ni mara nyingi sana unakuta mtu anapata kipato na
kuamua kutumia chote hasa mshahara akijua kwamba mwisho wa mwezi ataupata
mwingine,huyu hana tofauti na mvuvi mwenye imani na bahari bila kujali kwamba
kuna mawimbi, bila kujali kwamba kuna kukauka kwa mito na kupungua kwa kina cha
maziwa na samaki kuzaliana. Watu hawa mwisho wa mwezi unaweza kuwakuta wakiwa
hawana kitu na kuanza kuishi kwa kukopa. Yeye akipata hela hutumia katika kununua vitu ambavyo haviwezi kumzalishia mali. Mtu huyu ambae ni mvuvi hatakuwa na
uwezo wa kusonga mbele hata siku moja. Ataanzaje kwa mfano wakati hana mnyama
ambae kesho atazaa na kuwa nao wawili au watatu? Kama unataka kusonga mbele na
kufanikisha malengo yako ni muhimu uache kuwa mvuvi na kuamua kufuga, ni muhimu
kuana kujiwekea akiba. Kuna msemo wa kiingereza usemao ‘’A dollar saved is a
dollar earned’’ ukiwa na maana kwamba ‘’Dola moja iliyowekwa akiba ni dola
iliyokwishwa kupatikana’’.
Katika kitabu kitakatifu cha biblia, kuna mfano wa pacha wawili, mkubwa akiitwa Essau na mdogo akiitwa Yakobo. Essau alikuwa ni mwindaji na Yakobo alikuwa mfugaji. Siku ambayo baba yao alitaka kumbariki Essau alimtuma akawinde amletee nyama aweze kumbariki. Mdogo mtu na mamaye waliamua kumchukua mnyama ambae anafugwa na kumuandaa kisha kumpelekea baba yao Isaka. Mpaka muda huo Essau alikuwa ameshachelewa na hivyo kukosa baraka kutoka kwa baba yake. Laiti kama Esau angelikuwa na wanyama pale nyumbani pengine asingechelewa kupata baraka alizopanga kutoa baba yake kwake. Akiba aliyokuwa nayo Yakobo ilimfanya awahi fursa ya baraka. Ni mara ngapi umezikosa fursa muhimu kwa sababu ya kutokuwa na akiba? Unapokula kumbuka kuna kesho pia.
SOMA: Je mtaji ni kikwazo kwako katika kuanza biashara au kuwekeza?
SOMA: Je mtaji ni kikwazo kwako katika kuanza biashara au kuwekeza?
Kama utaamua kujiwekea akiba mathalani ya pesa ni
muhimu sana kuifanya iendelee kukua kwa
kuizungusha ili iweze kuzalisha nyingine. Mwadishi mmoja aliwahi kusumea kwamba
hela isiyozungushwa ni sawa na gazeti la zamani. Gazeti la leo halitakuwa na
thamani kesho ama kesho kutwa,matumizi yake ni leo tu. Huwezi kwenda kwa muuza
magazeti kununua gazeti la mwezi uliopita, kwanza ni vigumu kulipata. Akiba
utakayoipata iwekeze ili kipato chako kizidi kukua. Kila mara jiulize kama wewe
ni mfugaji au mvuvi. Acha kununua vitu ambavyo havikuzalishii chochote na uanze
kununua vitu vitakavyoongeza kipato chako. Watu ambao tayari ni matajiri na
wale wenye akili na mawazo ya kitajiri hawanunui vitu vya anasa kwa kipato au
mtaji wao bali kwa faida waipatayo kupitia vyanzo walivyovianzisha. Kwanini
umchinje ng’ombe mmoja ulienae kwaajili ya sherehe badala ya kusubiri umchinje
ndama wake? Kwa nini ufurahie kwa muda muda mfupi na kuteseka kwa muda wote
uliobakia? Kubali kuahirisha mambo yenye kusubiri kwa mambo yasiyoweza
kusubiri.
Pia katika mfano wa mfugaji na
mvuvi tunona tabia nyingine ya mvuvi ni kutokuwa na subira wala uvumilivu, yeye
anachojali ni kutuliza njaa yake ya leo. Wakati mfugaji anavumilia dhoruba
zitokanazo na mifugo yake. Anajua kuna magonjwa, njaa nk. Maana yake tunahitaji
uvumilivu ili kuweza kukua, huwezi kuzaliwa leo na kutembea kesho. Lazima
usubiri. Usione kwamba unapitwa, simamia katika malengo yako na usubiri huku
ukiendelea kuboresha mbinu zako za kongeza kipato. Usiogope kuanza na kitu
kidogo na kukua kuliko kusubiri mpaka kiwe kikubwa ndipo uanze, ukweli ni
kwamba hiyo siku haitakaa ifike. Mfugaji anaweza kuanza na kuku au ng’ombe
wawili na baada ya muda fulani akawa nao wengi wakati huo mwingine akisubri
apate pesa za kuanza na mia.
Nakushauri uwe na tabia za mfugaji kuweka akiba kisha kuwekeza katika vitu vyenye kuzalisha. Haiwezekani una vutu vyenye thamani kubwa ndani halafu huna uhakika wa kuishi ikitokea umefukuzwa au kusimamishwa kazi. Maisha ya ajira hayatabiriki hivyo anza kujiwekea akiba na kutafuta kitu cha kufanya. Vitu vyote vizuri utavinunua kwa faida na sio kwa mtaji. Matajiri unawaona walijinyima vitu vya thamani au anasa kwanza ili waweze kutengeneza mifereji ya utajiri.
Nina imani kuwa umenufaika na
makala hii. Wasambazie wale uwapendao.
Pia usisahau kupenda ukurasa wetu
wa facebook kwa kubonyeza hapa
na kujiunga na orodha yetu ya email kwa makala nzuri kila mara. Kwa makala za Afya na Lishe bonyeza hapa
Nickson
Yohanes
nmyohanes@gmail.com