Ndizi mbivu ni tunda lilotokanalo na mmea wa mgomba. Katika nchi yetu ya Tanzania kuna mikoa ambayo imebarikiwa kuzalisha ndizi kwa wingi. Mikoa hiyo ni Arusha, Kagera, Kilimanjaro, Mbeya na Morogoro. Ndizi zina rangi ya kijani zinapokuwa mbichi na njano zinapoiva na hivyo kuwa na rangi ya kuvutia. Ndizi pia zina ukubwa na maumbo tofauti tofauti. Ndizi mbichi hutumika kwa chakula kwa kupikwa na kuchanganywa na vyakula vingine kama nyama, maharage na samaki ila zikivumbikwa na kuiva hutumika kama tunda. Baadhi ya makabila hutumia ndizi mbivu kutengeneza pombe za asili kama lubisi na mbege. Pia kuna viwanda vya kisasa vinavyotumia ndizi kutengeneza mvinyo (wine). Kuna aina nyingi za ndizi lakini faida zake mwilini zinafanana.
Zipo faida kadhaa zinazotokana na ulaji wa ndizi mbivu. Faida hizo ni kama kudhibiti kiasi cha sukari mwili na pia kufanya mwili kutengeneza kemikali maalum za kufanya mwili kupumzika/kupunguza msongo. Faida nyingine ya ndizi mbivu ni uwezo wake wa kuweza kupunguza uvimbe katika sehemu ya mwili, kuzuia aina ya pili ya kisukari (type II diabetes), kupunguza uzito hasa kwa kuwa ndizi zina kiwango kikubwa cha nyuzi nyuzi (fibres), kuimarisha mfumo wa fahamu na kusaidia katika utengenezajiwa chembe nyeupe za damu (white blood cells) ambazo hupambana na magonjwa mwilini hasa kutokana na kuwa na kiwango kikubwa cha vitamini B-6.
SOMA: Namna bora ya kupungiuza uzito
SOMA: Namna bora ya kupungiuza uzito
Pia ndizi mbivu husaidia kupunguza sononeko (depression) kutokana na kuwa na kiwango kikubwa cha tryptophan ambayo hubadilishwa kuwa serotinin ambayo ni kihamasishi cha kutoa furaha katika ubongo. Mbali na faida hizo ndizi huoingeza nishati mwili kwa kuwa na wanga na sukari, huongeza damu kwa kuwa na madini ya chuma na hivyo kukuepusha na ugonjwa wa upungufu wa damu maarufu kama anaemia. Ndizi pia husaidia pia katika umeng`enyaji wa chakula (digestion) na kusaidia kupambana na sumu ziingiazo mwili kupitia vyakula mbalimbali.
Faida zingine zinazotokana na tunda hili maarufu ni husaidia kuupa utumbo afya kwa kuruhusu kuzaliana kwa bakteria wazuri ambao hufanya kazi mbalimbali mwili maarufu kama prebiotiki na husaidia pia katika utengenezaji wa vimeng`enyo kwaajili ya umeng`enyaji wa chakula mwilini. Kama vile haitoshi ndizi pia husaidia pia kupunguza maumivu ya vidonda vya tumbo kwa kufunika utumbo dhidi ya tindikali zichubuazo utumbo kama Haidrokloriki. Ndizi hutumika kupambana na kemikali zisizotakiwa mwilini au sumu (antiodixants) na pia kupambana na baadhi ya magonjwa sugu. Ndizi zina kiwango kikubwa cha madini ya magneziam na vitamini B ambayo husaidia kuacha uvutaji wa sigara.
Faida zingine ambazo hutokana na ndizi ni kusaidia afya ya akili hasa kumbukumbu na kujifunza, kusaidia tumbo kufanya kazi vizuri kutokana na kuwa na kiwango kikubwa cha cha nyuzi nyuzi (fibres), kupunguza kichefuchefu na kusaidia afya ya macho kwa kuzuia uharibifu wa misuli ya macho .Pia ndizi huzuia saratani ya figo na kuimarisha mifupa hasa kutokana na kuongeza uwezo wa mwili kuchukua madini ya kalsham kutoka kwenye vyakula vingine. Mwisho ndizi husaidia kurudisha chumvichumvi na sukari ipoteayo mwilini kutokana na ugonjwa wa kuendesha (diarrhea).
Naamini kuanzia sasa utaongeza ulaji wako wa ndizi mbivu ili kupata faida hizo zaidi ya kumi nilizoziainisha hapo juu. Kumbuka nyumba hujengwa kwa tofali, miti na zege lakini mwili wenye afya njema hujengwa kula vyakula bora.
Usisahau kumshirikisha mwenzako.
Makala hii imeandaliwa na kuandikwa na:
Nickson Yohanes
nmyohanes@gmail.com