Wanaobebeshwa lawama hizi, hawastahili kuzibeba

Malezi kwa watoto yamekuwa changamoto kubwa sana katika dunia hii ya sayansi na teknolojia tena dunia inayokwenda kwa kasi sana mithili ya roketi, dunia iliyojaa kila aina ya changamoto. Imekuwa ni kawaida sasa kusikia watu wazima wakiwalalamikia vijana ama watoto kuwa wamekuwa na tabia ambazo si nzuri hasa kulinganisha na wakati wao. Siwapingi lakini nani wa kulaumiwa, je mtoto, mzazi au jamii?.


Kabla sijamtaja mtu wa kulaumiwa (japo sishauri hivyo) nikumbushe kuwa mtoto huzaliwa akijua vitu viwili tu kulia na kunyonya na kuanzia hapo huanza kujifunza kidogo kidogo hasa kwa picha ama matendo. Baadae ataanza kujifunza maneno afikapo umri wa kuongea na hata kusoma na kuandika akibahatika kuhudhuria shule. Sasa swali la kujiuliza ni kwamba mtoto anajifunza haya kutoka kwa nani?. Bila shaka ni kutoka kwa watu waliomzunguka, baba, mama, wakubwa zake ,majirani,ndugu, jamaa na marafiki ambayo hiyo tunaita jamii yake. Katika jamii hii atajifunza mazuri na hata mabaya yaliyopo ndani ya jamii yake. Bahati mbaya au nzuri ni kwamba katika kipindi cha kujifunza mtoto hawezi kuchagua cha kujifunza na cha kuacha kwani hana uwezo huo. Pia ni kipindi ambacho yeye huwa na uwezo mkubwa wa kuhifadhi vitu vingi na pia kuwa uwezekano mdogo wa kuyasahau. Hivyo basi chochote ambacho mto huyu atajifunza basi kitanasa kichwani kwa muda mrefu na kiasi kwamba anaweza kufikia umri wa utu uzima na bado akaendelea kukumbuka yaliyotokea utotoni. Hivyo basi malezi ya mtoto hasa katika kipindi chake cha udadisi ni cha muhimu na inabidi jamii yake iwe makini kwani ndicho kipindi ambacho wanaweza kumtengeneza raia mwema ama raia mbaya wa Taifa husika, kipindi ambacho chaweza kumjeruhi mtoto husika.

Kama nilivyotangulia kusema katika aya iliyotangulia ni kwamba mtoto hujifunza kila kitu kutoka kwa watu waliomzunguka (jamii na wazazi) hivyo basi mtoto hapaswi kulaumiwa kwa tabia aliyo nayo bali kufundishwa na kuonywa ama kuadhibiwa inapobidi. Ni rahisi zaidi mtoto kujifunza kwa kuona kuliko kuambiwa. Mathalani mtoto amelelewa katika mazingira ya ubabe halafu wazazi au walezi wake wanamwambia kwamba awe mpole, haiwezekani!. Hawezi kujifunza asichokiona, hajui upole unafananaje na una faida gani. Mzazi kutwa unashinda kutakana watoto wako wanapokosea halafu utegemee watoto wako wasitukane watakapokosewa, itakuwa ni jambo gumu sana kwake maana ndivyo alivyofunzwa kuishi.

Mzazi jitahidi kuishi yale maisha ambayo utataka mwanao aje kuyaishi. Kama unapenda wanao wapende kusoma, basi kuwa mfano bora katika kusoma na sio kuishia tu kuwaamrisha kusoma. Mtoto hajawahi kukuona unashika kitabu hata cha dini yako halafu yeye kutwa unamhubiria kufanya hivyo. Nakuhakikishia atachukua kitabu na kukikodolea macho, kuhesabu kurasa lakini kamwe hatasoma na ukitoka tu na yeye ataweka kitabu chini. Tusiigize maisha, kama unapenda kuangalia TV tegemea hilo kutoka kwa mwanao pia. Kwani hujawahi kusikia watu wakisema `mtoto wa fulani yuko kama baba ama mama yake?´ Ni kwamba tabia za watoto ni picha ya familia wanazotoka, ni mabalozi wa familia zao popote watakapokwenda. Usiwe tabia zile ambazo hupendi mwanao awe nazo na hazikuwakilishi vyema katika jamii.

Changamoto kubwa iliyopo pia ni wazazi kutingwa na kazi (busy) kiasi kwamba jukumu la malezi limeachwa kwa msaidizi wa ndani maarufu kama yaya ama Housegirl kwa kiingereza. Kama msaidizi huyo akiwa na tabia njema anaweza kulea vizuri lakini japo sio jukumu lake kulea muda wote. Yeye anapaswa kukusaidia tu katika kipindi ambacho haupo nyumbani. Ukirudi kutoka kazini mlee mwanao walau ajue kwamba wewe ni baba au mama, watoto wengine wamelelewa na wasaidizi kiasi kwamba humsahau mama na kudhani wale wasaidizi ndio mama zao na mama zao huwaita dada, msifike huko. Tekeleza jukumu lako kama mzazi na kama ukiona haupo tayari kulea basi usiwe na mtoto mpaka utakapokuwa tayari kulea. Kama msaidizi akiwa na tabia mbaya (wakati mwingine kutokana na anavyoftendewa na bosi wake) basi mtoto huuvuna huo ubaya maradufu na hata wakati mwingine kudhuriwa. Kwani kesi kama hizo hujasikia? Zipo nyingi tu siku hizi. Sisemi usiwe na msaidizi wa kazi, bali usimwachie yeye jukumu la kulea peke yake, hilo ni jukumu lako wewe mzazi (baba na mama).

Pia nitumie fursa hii kukukumbusha tena kwamba ufanye yale ambayo unaona yanafaa kwa mwanao na atajifunza kutoka kwako na atakuwa mtu bora na raia mwema. Tabia nyingi alizonazo mtoto amezipata kwenye jamii yake. Na kama mtoto wako ataanza kuwa na tabia ambazo huzipendi na wewe huzifanyi, tafuta chanzo cha tabia hizo mfano udokozi, matusi na tabia zinazofana na hizo na kumtenga na chanzo hicho kama hatua ya kwanza na pia kumkanya hata kumuadhibu pale inapobidi ili ajue kuwa kafanya kosa alijutie kosa hilo. Kwa wasomaji wa Biblia watakubaliana na mimi kuwa kuna mstari unaosema mlee mtoto katika njia impasayo naye hataiacha hata atakapokuwa mzee. Pia kuna msemo wa Kiswahili usemao mtoto umleavyo ndivyo akuavyo. Ukimlea vyema atakua vyema na ukimlea vibaya atakua vibaya. Usikubali mwanao awe balozi mbaya kwako na usiubali apatikane raia mbaya wa nchi yako. Jamii yetu isikae kimya na kushindwa kukemea mabaya ambayo wanayaona kwenye malezi ya watoto wa jamii zetu. Mke wa rais mstaafu wa awamu ya nne aliwahi kusema Mtoto mwenzako ni wako, na wa kwao pia ni wako. Kwa pamoja tuwalee ili tujenge taifa bora la sasa na la baadae. Mzazi usichukie pia pale mwanao atakapoonywa ama kuadhibiwa kwa makosa aliyofanya. Cha muhimu adhabu isiwe ndiyo kitu cha kukimbilia mtoto anapokosea, mpe elimu kwanza na akikaidi basi adhabu inayolingana kosa alilotenda itolewe. Usimlee kama yai,mlee kama mtoto. Kina baba jukumu la kulea ni la wazazi wote, baba na mama.
Mzazi, mlezi,ndugu jamaa, jamaa, marafiki na jamii kwa ujumla ni jukumu letu sote kulea na tunapaswa kulaumiwa sisi kwa tabia mbaya watakazokuwa nazo watoto waliopo katika jamii zetu.

Ni mategemeo yangu kwamba kwa pamoja tutajenga jamii imara na kuopata raia bora wa leo na hata kesho. Acha alama bora kwa mwanao ambayo kamwe haitafutika na atairithisha kwa wajukuu zako na hata kizazi chako chote.

Nina mengi ya kuandika lakini niishie hapa kwa leo. Tukutane katika makala zijazo, siku njema!.

Nickson Yohanes
nmyohanes@gmail.com
07538430303/ 0712843030

Related Posts