Je umepanda nini shambani kwako?

Habari za muda huu ndugu msomaji wa mtandao huu.
Kuna misemo mingi sana katika lugha ya Kiswahili na mmojawapo wa msemo huo ni memo usemao kwamba akipandacho mtu ndicho atakachovuna. Waliosema hivyo waliona mbali sana na msemo huu una ukweli ndani yake.


Kama swali lilivyouliza hapo juu ni dhahiri kwamba utavuna kitu chochote ambacho wewe utakuwa umepanda na sio vinginevyo na uzuri au ubaya wake ni kwamba utavuna maradufu. Mathalani ukipanda mbegu moja ya mwembe katika mazingira mazuri basi nayo itaota na kukupa idadi kubwa ya maembe. Je ukipanda maembe unaweza kutegemea kuvuna mapapai? Ama ukipanda maharage utavuna dengu? Jibu ni hapana utavuna sawa sawa na ulichokipanda wewe.

Nirudi kwenye swali la msingi sasa ni kwamba kila mtu anatakiwa kupanda kile ambacho atataka kukivuna baadae, mathalan kama unataka kupanda upendo huna budi kupanda upendo, kama unataka kupanda kuvuna amani huna budi kutenda haki katika maamuzi unayoyafanya. Hebu tuchukulie kwamba umepanda mbegu ya chuki hakika utavuna chuki maradufu. Huwezi kuvuna usichopanda hilo usilitegemee kamwe. Kama unataka kuwa tajiri huna budi kupanda juhudi na maarifa ambayo itaongeza thamani katika kile unachokifanya, na ukitaka kuwa na familia bora huna budi kuwekeza katika kupenda na kuijali familia yako. Kama unataka kupokea yakupasa pia kutoa, kama unataka afya bora huna huna budi kufuata kanuni bora za afya na mengine yahusuyo afya. Tatizo kubwa ambalo watu wengi wanalipata ni pale wanapoanza kupanda na kutegemea mavuno ya haraka katika muda mfupi tokea kupanda. Lazima usubiri kipindi cha mavuno kifike, mazao yako yakomae pia.

Labda nikuulize swali ndugu msomaji, mtu apandapo mahindi anaweza kuvuna ndani wiki? Ama apandapo minazi anaweza kupata nazi baada ya mwaka? Jibu ambalo nahisi utakuwa umelijibu ni kwamba haiwezekani na ni lazima kusubiri wakati unaendelea kutunza mazao yako shambani vile vile ndiyo hivyo utakavyoendelea kupalilia uyatakayo hata kama mazao bado hayaonekani. Hakuna mama anaetaka mtoto ambae atashindwa kusubiri miezi tisa, akishindwa kusubiri basi hatapata mtoto bali atapata njiti. Pia unatakiwa kupamda mbegu zako unazotaka kuvuna katika mazingira mazuri ambayo yataleta mazao mengi na bora. Mazingira hayo ni pamoja na kuwa na imani kwamba utavuna, kama huna imani kwamba utavuna hutakuwa na hamasa ya kutunza mimea yako.

Ndugu msomaji wangu nakushauri upande mazao bora tena ambayo utaweza kuvuna kwa muda mrefu japo yatahitaj pia muda mrefu kukua na kumea. Mkulima wa mchicha hupanda mbegu na kuvuna ndani ya muda mfupi lakini hataweza kuendelea kuvuna kwa kipindi kirefu, lakini mkulima wa minazi husubiri sana lakini siku akianza kuvuna atavuna kwa muda mrefu sana pengine kizazi hadi kizazi. Panda tabia njema na utavuna heshima, panda chuki na utavuna chuki, panda mema na utavuna mema, lea vizuri na tunza vyema familia yako na wewe utapata familia bora na yenye upendo, amani na heshima, saidia nawe utasaidiwa, hudumia nawe utahudumiwa. Watendee watu yale ambayo nawe utataka kutendewa na kamwe usimtendee mtu jambo ambalo wewe hutaki kutendewa. Kumbuka kila siku ni msimu wa kupanda.
Amua leo utapanda katika wema na wewe utavuna kwa wakati wake tena utavuna maradufu.

Nikutakie mafanikio tele.

Nickson Yohanes
0753843030 au 0712 843030

Related Posts