Choma meli yako sasa

Ndugu msomaji napenda kutumia wasaa huu kuweza kukusalimia kabla sijaanza kukushirikisha niliyonayo leo. Nianze kwa kukusimulia hadithi moja:

Hapo zamani kuna kiongozi wa nchi fulani alienda vitani na jeshi lake katika nchi ya kigeni kwa kutumia usafiri wa meli. Alipofika pwani ya nchi ya adui aliamuru jeshi lake kuchoma meli waliyokwenda nayo. Aliwaambia wapiganaji wake kwamba kwa sasa wana machaguo mawili tu ambayo ni kushinda ile vita na ni lazima washinde ama kufa wote kwani hawawezi kutoka salama huko kwa kutoroka kwani wameshachoma moto meli yao. Wasiposhinda maana yake watauawa ama watakuwa mateka ama washinde vita na warudi nchini kwao salama. Hapo sasa kukawa hakuna jinsi zaidi ya jeshi lake kuwa na dhamira moja tu ya kushinda kwani kwani kwa namna yoyote hawako salama maana wakipigana wanaweza kushinda lakini pia wanaweza kufa na wasipopigana pia wanaweza kufa kwa hiyo walijitoa kwa
moyo mmoja na kuamua kupambana na adui. Walishikamana na kuamua kupambana na kwa moyo mmoja na hatimaye wakashinda ile vita. Bila wao kudhamiria kushinda ile vita kamwe wasingeweza kushinda, bila kuchoma meli yao naamini wasingeweza kuishinda vita ile. Kuchoma ile meli ndiyo maamuzi magumu waliyoyafanya na kuamua kuishinda. Kuna kiongozi wa Tanzania aliwahi kusema ``Ni bora kulaumiwa kwa kuchukua maamuzi magumu kuliko kulaumiwa kwa kutokuchukua maamuzi magumu.´´


Hadithi hii inatufundisha nini mimi na wewe? Hadithi hii inatupa funzo kwamba ili ushinde kitu chochote katika maisha haya ni lazima kuwa na nia ya dhati ya kushinda. Hutakiwi kusitasita pale utakapokuwa na nia ya kufanikiwa. Dhamira ya ushindi iliyokuwapo kwa kamanda wa vita mpaka kuamuru kuchoma meli yao ndiyo ambayo inatakiwa kuwa kwako kama unataka kufanikiwa. Ni vigumu sana kupata mafanikio kama hutadhamiria kufanikiwa, ni vigumu pia kushinda kama hutajitoa kujiletea mafanikio bila kujali vikwazo vilivyoko mbele yako. Kuendelea kusita kutaendelea kukuzuia kuchukua hatua na mara nyingi utakuta unaaihirishisha kabisa ama kufuta lile ambalo umedhamiria kulifanya.
SOMA: Je umepanda nini shambani kwako?

Unatakiwa udhamirie kufanya kile ambacho unataka kufanya. Lazima pia uamini kwamba utashinda kwa namna yoyote ile. Lazima ujitoe sadaka kwa kweli maana mafanikio yangekuwa yanakuja kirahisi basi kila mtu angekuwa amekwisha kufanikiwa. Bila kuchoma meli yako hakika huwezi kushinda vita vya mafanikio. Mafanikio lazima uyatafute kila siku, ni safari ya maisha yako.

NInaposema mafanikio simaanishi mafanikio ya kipesa ama utajiri pekee bali namaanisha mafanikio katika nyanja zote kama afya, elimu, biashara na kila kitu ambacho wewe unakifanya. Kwa mfano kama ukitaka kuwa na afya njema lazima ujitoe kula vizuri, kufanya mazoezi, kupima afya na hata usafi pia. Si rahisi sana kama ambavyo wengi wanavyochukulia maana kuna wakati utalazimika kula ambacho hukipendi ama kufanya ambacho hukipendi pia. Kwenye mafanikio ya kipesa mfano ni lazima mtu afanye kazi kwa bidii na maarifa, ajinyime baadhi ya vitu, ajitolee kujifunza mara kwa mara na pengine ni kila siku na hata kuingia gharama kubwa tu ili afanikiwe.

Ndugu yangu meli yako ipeleke kwa adui yako na kisha uichome moto. Meli yako ni kile kituambacho kinakufanya usijitoe kufikia mafanikio, Kama ni uvivu basi choma moto, kama ni tamaa, kuwaza kushindwa , maarifa duni, afya mbovu na yote yanayofanana na hayo. Huna budi kuichoma moto meli iliyobeba vitu hivyo na kubaki na nia na dhamira ya kweli ya wewe kufanikiwa. Kama umekuwa ukipanga jambo na umeshindwa kulifanya ni muda sasa wa kuanza kulifanya kwa moyo wote bila kusitasita.

Naamini utajifunza na kuweza kufanyia kazi haya ambayo umeyajifunza leo. Kumbuka kwamba 
huwezi kufanikiwa kwa kusoma tu bila kuyafanyia kazi uliyoyajifunza. Mtu mmooja aliwahi kusema kwamba huwezi kujifunza kuogelea kwa kusoma kitabu. Ni lazima uingie majini na kuanza kuogelea. Japo utakosea lakini hatima yake ni kuweza kuogelea.

Washirikishe wenzako makala hii:

Nickson Yohanes
nmyohanes@gmail.com

Related Posts