Habari za wakati huu ndugu msomaji wa makala zangu katika mtandano huu wa PAMBAZUKA DAIMA ni matumaini yangu kwamba uko bukheri wa afya, na kama kwa vyovyote vile hali yako ya kiafya siyo ya kuridhisha basi nakupa pole na kukuombea upate nafuu na upone haraka.
Ndugu msomaji kumekuwepo na tabia ya watu wengi kupuuzia vitu ambavyo vina madhara kidogo ama ambavyo huchukua muda mrefu kuliko vile ambavyo vinaonyesha madhara katika muda mfupi. Vitu ambavyo vinasababisha ugonjwa papo hapo ama baada ya muda mfupi huchukuliwa kwa umakini mkubwa kulinganisha ni vile ambavyo vinachukua muda mrefu kusababisha ugonjwa.
Leo ningependa kidogo kuzungumzia vifungashio (packages) vya vya chakula ambavyo vimekuwa vikitumiwa na wetu wengi hasa kubebea vyakula vya moto kama chipsi. Vifungashio hivyo si vingine bali ni mifuko ya plastiki maarufu kama mifuko ya rambo. Ukiangalia kwa jicho la kawaida hutaweza kuona madhara yake moja kwa moja hasa kutokana na kwamba huchukua muda mrefu kuja kuona madhara yake ni hivyo watu wengi kutokutilia maanani na mazoea pia ya matumizi ya mifuko hiyo kwenye jamii zetu.
Mitaani na maeneo hasa ya vyuo vikuu kumekuwa na mazoea ya kubeba vyakula vya moto hasa chipsi wakiwa na lengo la kwenda kulia sehemu nyingine mbali na sehemu vinapouzwa.
Mifuko ya plastiki inapopigwa na joto mkali au mdogo kwa muda mrefu hutoa kemikali ambazo huingia kwenye chakula na hivyo kuingizwa mwilini kwa njia ya kula. Kama kemikali hizo zitaendelea kuingizwa kwenye mwili zitaendelea kujijenga mwilini na hivyo kumuweka mlaji katika hatari ya kuugua ugonjwa wa saratani (kansa). Ugonjwa wa kansa kama mjuavyo hauwezi kuanza kama malaria bali huanza kidogo kidogo na mpaka uje kuonekana basi utakuwa umeshambaa sana mwilini. Hatari iliyopo katika mifuko hii si kwa vyakula vya baridi bali vyakula vya moto ambavyo hufanya kemikali hizo kuyeyuka na kuingia kwenye chakula. Kemikali hizo zinajulikana kama Polyvinyl Chloride, polyethylene, polystyrene, styrene na bisphenol.
Mbali na kuongeza uwezekano wa kuugua saratani pia madhara mengine yanayohusishwa na matumizi ya mifuko ya plastiki kubebea vyakula vya moto ni kubadilika kwa jeni za mwili, kuharibika kwa jeni za mwili, matatizo ya uzazi, matatizo ya moyo na matatizo ya kushindwa kuweka katika msawazo (urari) vichocheo mbalimbali vya mwili (homoni) ambavyo husaidia ufanyaji bora kazi wa mwili na hivyo kuathiri baadhi ya tabia hasa kwa watoto.
Kama hakuna ulazima wa wewe kutumia mifuko ya plastiki kubebea vyakula vya moto basi acha kabisa maana matumizi yake. Wahenga walisema ´bora kinga kuliko tiba´, hivyo basi ni bora kuzuia tatizo linalozuilika sasa ili kuepuka madhara ya kesho. Ni imani yangu kwamba utaweza kupunguza matumizi ya mifuko ya rambo katika kubebea vyakula vya moto na hatimae kuacha kabisa. Najua sio jambo rahisi hasa kama umeshazoea lakini ukiamua utaweza kabisa kuacha matumizi hayo.
Nikutakie utekelezaji mwema.
Nickson Yohanes
Email: nmyohanes@gmail.com