Ili uweze kupata mafanikio ni lazima ulipe gharama hizi

Habari za muda huu ndugu msomaji wa mtandao huu wa PAMBAZUKA DAIMA, natumaini kuwa hujambo na unaendelea vyema na harakati za kujiletea maendeleo , kama hauko vyema basi pole na kumbuka kuwa hizo ni changamoto za maisha ambazo tunazipitia.

Je unalipa gharama za mafanikio?
Hili ndilo swali ambalo unatakiwa kujiuliza kabla hujaendelea mbele, kisha fuatana nami hapa chini ili tusome kwa pamoja.
Neno mafanikio ni neno linalovutia sana kulisikia masikioni, najua kwanini ni kwa sababu kila mtu ananyatamani na kuwaza kuyafikia mafanikio. Kuna mafanikio yapo katika nyanja zote kama afya, elimu, fedha na hata kiroho. Mafanikio huja kwa njia nyingi na namna mbali mbali lakini kuna kanuni kubwa ya kuweza kufanikiwa. Kanuni hiyo ni kulipa ghara za kufanikiwa. Hakuna yeyote alieyewahi kufanikiwa bila kulipa gharama zinazotakiwa kuweza kufanikiwa. Kama unataka kufanikiwa basi kuwa tayari kulipa gharama hizo. Wengi hujaribu kukwepa kulipa gharama na kuamua kutumia njia ya mkatio ya kutafuta mafanikio. Ukweli ni kwamba hakuna njia ya mkato bila kulipa gharama, na mara nyingi ukijaribu kukwepa gharama utajikuta unalipa gharama kubwa sana baadae.


Miongoni mwa gharama za kulipa ni muda wako. Ni lazima uwekeze muda wako katika kile ambacho unakifanya. Kwa mfano kwa mwanafunzi itamlazimu yeye kuutumia muda wake mwiingi kwa kusoma na kujiandaa na mitihani na kwa upande wa mkulima atautumia muda wake mwingi kuhudumia shamba lake. Lazima uutenge muda wa kutosha kwa shughuli ama jambo lile ambalo umepanga kulifanikisha. Tumia muda wako vizuri maana huwezi kuulinda muda bali unaweza kuutumia vyema, kumbuka tu kwamba kila mtu ana saa 24 tu na hakuna mwenye zaidi ya hapo. Matumizi mazuri ya muda wako kwa kuwekeza katika kile cha kuweza kukuletea mafanikio ndiyo yatayokutofautisha wewe na wale ambao hawajafanikiwa. Usiutumie muda wako katika vile vitu ambavyo si muhimu na havikusaidii kusonga mbele kuelekea kwenye mafanikio kama muda mwingi wa kupiga soga, kutumia muda mwingi katika mitandao ya kijamii na kuzurura.

Gharama ya kufanya kazi kwa juhudi na maarifa, huu ni ukweli ambao lazima sote tuujue. Huwezi kufanikiwa kama hufanyi kazi, tena ufanye kazi kwa juhudi na maarifa. Sio nguvu peke yake bali maarifa pia lazima yawepo maana kuna watu wengi sana ambai ni hodari wa kufanya kazi lakini ni masikini wa kutupwa. Lazima ujue ni wapi hasa pa kuwekeza juhudi zako. Mbali na hilo ni lazima pia ujiongezee maarifa kupitia njia mbalimbali mfano kusoma sana vitabu. Maarifa mengi tuyatakayo yapo kwenye vitabu, yameshaandikwa tayari. Pia kuhudhuria semina na matamasha yanayokuongezea maarifa katika kile unachofanya. Kwa mfano wewe ni mfanyabiashara unaweza kuhudhuria semina za kukuza mitaji, uwekezaji na hata mauzo.

Uvumilivu ni gharama nyingine ambayo unatakiwa kuilipa. Kama ukitaka kufanikiwa kweli ni lazima uweze kulipa gharama hii. Uwezo wa kuweza kuvumilia ndio utofauti wa kipekee uliopo miongoni mwa waliofanikiwa na wasiofanikiwa. Watu wengi wenye kuvumilia kuyasubiri mafanikio huku wakiendelea kujituma ni dhahari kuwa watafanikiwa. Usiwe na tamaa ya kupanda na kuvuna kesho, Mfikirie mkulima wa miti ambae hupanda miti na kusubiri zaidi ya miaka minane, kama sio mvumilivu asingeweza kuipanda miti hiyo. Kuna dhoruba nyingi kufika huko lakini huna budi kuvumilia kama kukatishwa tamaa, kuanguka na kadhalika lakini huna budi kufika kileleni. Kumbuka tena hakuna njia rahisi wala ya mkato ya kuyafikia mafanikio isipokuwa kwa kuilipa gharama. Jiwekee lengo kwamba utafanikiwa na lazima utafanikiwa tu.

Gharama za fedha, fedha ni muhimu sana tena sana. Pesa ni mtumishi mwema sana ambaye anaweza kukufanyia kazi zako na kukuletea faida. Hakuna mtu hata mmoja ambaye anasema pesa sio muhimu. Utahitaji fedha ili uweze kuwekeza, kufanyia biashara, kuisha na mengine mengi ambayo unayajua kuhusu fedha. Kuwa tayari kulipa gharama za kifedha kuweza kufanikiwa. Wekeza pesa ili uweze kufanikiwa ili uweze kupata faida pia.

Kujitoa sadaka (self-sacrifice), Hili ni la lazima sana kuweza kufanikiwa. Hakuna njia nyingine ndugu lazima ujiotoe sadaka, lazima ukubali kuyasotea mafanikio yako. Mwanzoni mambo huwa magumu sana hata kukufanya ukate tamaa. Uvumilivu na imani kubwa ni muhimu sana kwa kipindi hiki. Bondia maarufu sana dunia marehemu Muhammad Ali aliwahi kusema ``Niliichukia kila dakika ya mafunzo lakini nikasema ´Usiondoke´Teseka sasa ili uishi maisha yako yote kama mshindi´´. Ni lazima ujitoe kweli kweli, ni lazima uamue kutafuta kile unachokitaka. Mafanikio sio rahisi ndio maana sio watu wengi wamefanikwa. Ni lazima uamke mapema, ni lazima ufanye kazi hata kama hupendi, lazima kujifunza, lazima uchelewe kulala wakati mwingine, kujinyima baadhi ya vitu, kutokubali kukatishwa tamaa na vingi vingine.

Upendo nao ni gharama nyingine ya kulipa, unaweza kuiona ndogo lakini si kweli. Utahitajika kuwapenda maadui zako, wabaya wako, washindani wako na hata washindani wako. Utahitaji kuwapenda watu ili ujifunze kutoka kwao, sio upendo wa usoni tu bali ni upendo kutoka moyoni. Yakupasa pia upende unachokifanya, ukipenda unachokifanya utakifanya kwa moyo wako. Kama bado hujapata unachokipenda jaribu kukitafuta. Hata kama mtu anakuchukia sio lazima na wewe umchukie.

Kufanya vihatarishi (Take risks), watu wengi wanaogopa kuthubutu. Wanaogopa kujaribu kufanya kitu kipya kwa kuhofu kuhusu hatari zilizopo katika kitu hicho. Wako tayari kuendelea kuwa katika hali waliyonayo badala ya kujaribu kuchukua hatua. Ni bora zaidi kufanya kitu cha kuhatarisha kuliko kukaa bila kufanya chochote.Ni hatari zaidi kukaa bila kufanya vihatarishi kuliko kufanya. Watu wengi hawajutii vile vitu ambavyo wamevifanya hata kama walishindwa bali vile ambavyo hawakufanya. Utafiti uliofanyika unaonesha kwamba wale watu wanaothubutu kufanya vitu vya hatari hushindwa mara chache zaidi kuliko kufanikiwa.

Katika vita vya pili vya dunia marubani wa ndege za kivita waliokuwa tayari kukabili hatari waliweza kuokoa maisha yao kuliko wale ambao walikuwa wakijihami zaidi na kuogopa kukabili hatari. Utafiti mwingine unaonyesha kwamba wale watu ambao huishi kwa tahadhari sana huishi muda mfupi kuliko wale wanaojiingiza katika hatari. Kufanya vitu hatarishi haimaanishi kufanya vitu vya hatari ovyo, siku zote fanya hatari ambazo umeshazipigia mahesabu, Waingereza wanasema take calculated risks.
Nakuatakia utekelezaji mwema.

Nickson Yohanes
Email: nmyohanes@gmail.com

Related Posts