Umezungukwa na watu wa aina gani?

Habari za muda huu ndugu msomaji wa mtandao huu wa PAMBAZUKA DAIMA. Ni matumaini yangu kwamba unaendelea kusonga mbele licha ya changamoto za hapa na pale unazokutana nazo, changamoto hizo ni magurudumu katika safari yako. Kwa wale waliokuwa wananifuatilia hapo zamani watakumbuka kuwa nilikuwa naandika kupitia blog ya Life Adventures ambayo nimehamishia makala zote huku na kwa wasomaji wapya nitumie fursa hii kuwakaribisha.

Ndugu msomaji katika hii dunia tumezungukwa na vitu mbalimbali. Tumezungukwa na watu, vitu, mimea na hata wanyama. Vitu hivi vyote vinaweza kutuathiri kwa namna hasi au namna chanya. Tunaweza kuathiriwa zaidi na binadamu wenzetu kuliko tunavyoweza kuathiriwa na vitu vingine. Lakini pia sio kila binadamu anaweza kutuathiri bali wale ambao tunatumia muda wetu mwingi nao. Hao si wengine bali ni ndugu,jamaa na marafiki. Ndio, hao ndio watu ambao mara nyingi tunapendezwa nao na hivyo kujikuta kwamba tuko nao muda mwingi sana kiasi cha kuweza kutuathiri. Kuna msemo wa Kiswahili usemao kwamba unaweza kuchagua marafiki lakini huwezi kuchagua ndugu na majirani. Huu msemo uko sawa kabisa kwani kama ndugu zako si watu wazuri huwezi kuwakataa kuwa si ndugu zako, vile vile unaweza kuwa na majirani wabaya sehemu unayoishi sasa ama ukajikuta kwamba kila unapohamia unakutana na watu wa ajabu tu. Sote tuna uwezo mmoja mkubwa wa kuchagua marafiki, ndio marafiki tunaoona tunaendana nao, marafiki ambao tabia zao zitatujenga kuliko kutubomoa. Labda sisi tuliopo katika kizazi hiki cha teknolojia tuna nafasi kubwa ya kuathiriwa hata na watu tusiowafahamu kuliko vizazi vilivyotutangulia hasa kupitia mitandao ya kijamii kama facebook, whatsapp, telegram, tweeter,instagram nk. Tunaweza kujaza hisia hasi ama chanya kwa haraka zaidi kuliko kipindi chochote kingine katika historia ya dunia hii. Bahati mbaya ni kwamba wengi wamekuwa wakitumia mitandao hii kwa kubomoa zaidi kuliko kujenga. Ni muda sasa wa wewe kutafakari aina ya makundi ya kijamii ama watu waliopo mitandaoni unaowafuatilia. Usikae katika kundi au mtandao wa kijamii usiokujenga,bali kaa sehemu ambayo unaweza kuambukizwa chaji chanya za maisha.

Tabia za watu wengine huathiriwa zaidi na tabia za marafiki zao au watu anaotumia nao muda wake mwingi. Kama utakuwa na marfiki walevi bila shaka nawe utakuwa mlevi, ukiwa na marfiki wezi nawe utakuwa vile vile, ukiwa na marafiki wenye mafanikio nawe pia utakuwa na mafanikio na hata pia ukiwa na marafiki walalamikaji nawe utakuwa mlalamikaji vile vile. Unaweza kupingana nami lakini ukweli ni kwamba ndege wafananao huruka pamoja.Mafanikio yetu ni wastani wa watu wa tano tunatumia muda wetu mwingi na wao. Mbuzi hawezi kukaa na mnyama mwingine muda mrefu kama afanyavyo kwa mbuzi mwenyewe. Tabia za watu walikuzunguka zinaakisi tabia zako. Kama watu hawana uhakika na tabia zako basi wataangalia tabia za marafiki zako, hii ni kwa sababu mtu huvutiwa na tabia za wanaomzunguka. Ndugu, jamaa na marafiki wana nafasi kubwa sana ya kutuathiri na kutufanya tufanikiwe ama tusifanikiwe katika kile tunachokifanya. Kama una marafiki wakatishaji tamaa nawe utakuwa mkatishaji tamaa ama mkata tamaa mwenyewe. Marafiki hasi na walalamikaji watakufanya kuwa mmoja wao na sio tofauti nao, marafiki waoga huwa na marafiki waoga ama ambao wataambukizwa tabia hizo za uoga.

Ni muda sasa wa kutathmini aina ya watu wanaokuzunguka kama ni watu wanaokusaidia kusonga mbele ama kurudi nyuma. Kama ni kundi la kukupeleka mbele basi unaweza kuendelea nao na kama ni wa kukurudisha nyuma,acha kutumia muda wako mwingi na wao. Sijasema uwatenge la hasha ila kupunguza ukaribu nao na utafute marafiki wenye malengo sawa na yako, marafiki chanya na marafiki wenye msaada kwako kwa namna moja au nyingine. Kama ni ndugu najua kabisa huwezi kuwakataa kwamba sio ndugu zako bali cha kufanya ni kutokaa nao muda mrefu kiasi cha kukuathiri, unaweza kutumia muda mfupi tu kujuliana hali ama kujadili masuala muhimu ya familia pale inapobidi. Tafuta watu werevu kama wewe au kuliko wewe, ambao unaweza kujifunza kutoka kwao. Kuna mtu aliwahi kusema kwamba kama katika kundi wewe ndiye mtu mwerevu pekee basi ni muda wa kuliacha hilo kundi na kutafuta kundi lingine. Hii ni kwa sababu badala yaw ewe kujifunza kutoka kwao utaweteka na kujisahahu ama kujiona wewe ndio kila kitu na kubweteka na huku pia jamaa hao wakikunyonya badala ya kusaidiana. Usiogope kuwapoteza marafki ambao wanakuvuta kuelekea nyuma, marafiki waliojaa mawazo hasi au marafiki wanaokunyonya,siku zote kuwa na watu mtakaofaidishana (win-win situation). Utapata marafiki wengine bora zaidi.

Kumbuka kwamba marafiki na watu walikuzunguka wana nafasi kubwa ya kuamua kiasi cha mafanikio yako, ni lazima uchukue hatua mara moja kabla hujachelewa. Tafuta watu chanya, watu wenye kukusongesha mbele, watu wenye kutia moyo na watu wenye kukusaidia pale unapohitaji msaada wao au watakapoona unahitaji msaada. Kuna marafiki wanawaza kukata tamaa muda wote, wegine wanawaza starehe muda mwingi na wengine wanawaza kuhusu namna ya kufanya makubwa. Ni heri uwe peke yako kuliko kuwa na marafiki hasi. Kubali ukatae ukikaa na kundi lolote nililotaja utaanza kuzoea (adapt) hali hiyo na kuona ni kawaida. Unadhani watu wengi wameanza kunywa pombe, kuvuta bangi na sigara, ujambazi na tabia zinazofanana na hizo kupitia nani kama sio ndugu, jamaa na kwa kiasi kikubwa sana marafiki? Ni vigumu kukutwa kwenye kundi la majambazi halafu watu wakaamini kwamba wewe sio jambazi.

Marafiki wawe chachu ya wewe kusonga mbele na sio kukurudisha nyuma. Watu waliofanikiwa hukaa na watu waliofanikiwa. Watu wasiofanikiwa hukaa na watu wasiofanikiwa, hawachangamani kama ilivyo kwa mafuta na maji. Kuna msemo wa KIkemia usemao ‘’Like dissolve like’’ ukiwa na maana kwamba vitu vinavyofanana huyeyushana kwa vyenyewe mfano maji kwa maji na mafuta kwa mafuta. Hivyo hata kama hukuwa na tabia fulani utaambukizwa kutoka kwa marafiki zako. Kulikuwa na jamaa ambae kila mwaka mpya wa masomo ukianza alipokuwa anasoma alikuwa akiwaambia watu kuwa baadhi ya masomo ni magumu sana na uanaweza kufeli, ama mwalimu fulani ni mbaya. Unajua kilichotokea? Ni kwamba maneno yake ya kukatisha tamaa na ya kujirudiarudia yaliwaingia baadhi ya watu moyoni na kwenye akili na kutengeneza ugumu wa masomo husika ambayo hatima yake ni kwamba walifeli masomo husika. Ugumu aliouona yeye aliwaambukiza marafiki zake. Sio tu kwamba aliwaambukiza tabia hiyo bali pia tabia zingine ambazo pengine zisingefaa kwenye jamii iliyostaarabika. Kila mtu ana rafiki, ndugu au jamaa ambae amemgusa kwa namna moja ama nyingine iwe hasi au chanya. Kila mtu anaweza kutoa mfano wa rafiki yake mwenye tabia fulani kama akipewa nafasi. Ni muda wa kukaa mbali na rafiki mwenye tabia kama nilizotaja kwenye mfano ama ubaki nae uangamie.

Kama kuna mtu ambae alikuwa masikini na kushinda maskani ama kijiweni, siku akianza kufanikwa hupata marafiki wenye mafanikio ama alihama kuwatafuta watu wenye mafanikio wenzake. Ni vigumu sana kuwakuta matajiri katika vijiwe vya masikini na hii hupelekea masikini au watu uliokuwa nao kijiweni kusema kwamba umeanza kuringa baada ya kuanza kutajirika, unakumbuka ‘’like dissolve like?’’. Siku alifanikiwa akianza kurudi kijiweni kukaa na wale watu wenye mawazo hasi, kuna mawili yanweza kutokea nayo ni yeye kuwapandisha kwa kuwabadili ( na inaweza kuwa ngumu pia) ama yeye kurudishwa nyuma ili aweze kufanana nao. Badili marafiki kabla hajakubadili wewe,badili maisha yako.

Wajali ndugu,jamaa na marafiki zako kwa kuwatumia makala hii. Pia usisahau kujiunga nasi kwa email ili kupata makala na vitabu na kuLike page yetu Facebook kwa kunyeza hapa. Kupata makala za Afya,Chakula na Lishe bonye za Hapa
Nickson Yohanes

nmyohanes@gmail.com

Utofauti mmoja mkubwa uliopo baina ya mfugaji na mvuvi

Hbari mpendwa msomaji wa mtandao huu wa PAMBAZUKA DAIMA ni matumaini yangu kwamba unazidi kulisongesha gurudumu la kuelekea kwenye mafanikio ya maisha yako.

Leo ningependa nikushirishe kuhusu utofauti mmoja uliopo kati ya mfugaji na muwindaji au mvuvi.
Sote tunajua kuwa jamii zote hizi nilizojata zinategemea wanyama kwaajili ya kuendesha  maisha yao, wafugaji wakiwategemea wanyama wawafuagao huku wavuvi wakitegemea kuendesha maisha yao kwa kuvua samaki na wawindaji wao wakitegemea kuwinda wanyama wa porini kuendesha maisha yao. Japo jamii za uwindaji zinaonekana kama zimekwisha katika karne hii bado kuna jamii chache sana zinazotegemea kuishi kwa kutegemea uwindaji.

Mfugaji ni yule mtu anaefanya kazi ya kuwatunza wanyama na kuwafanya waongezeke maradufu. Huwawekea mazingira mazuri ya kuishi, matibabu na malisho. Huishi kwa kuwategemea kwa chakula hasa maziwa na nyama. Muwindaji hachinji wanyama wake ovyo bali huwachinja kwa utaratibu maalum tena baada ya kuongezeka sana. Umeshawahi kumuona mfugaji mwenye ng’ombe mmoja akaamua kumchinja? Jibu ni hapana. Kitu kingine ni kwamba wafugaji wengi huwapenda sana mifugo yao kiasi kwamba hawawachinji au kuwauza mara kwa mara. Ni kutokana na tabia hii ya wafugaji kujikuta wana mifugo wengi. Mifugo ninayoizungumza ni ile mifugo ya kawaida ambayo hata Tanzania tunao kama ng’ombe, mbuzi, kondoo, kuku na hata samaki. Hivyo basi tabia ya mfugaji tunayoiona hapa ni kusubiri kula mazao yatokanayo na mifugo yake na sio kula mifugo yake kabla haijazaliana.



Kwa upande wa muwindaji au mvuvi yeye anaamini kwamba pori, ziwa, mto au bahari zipo tu na samaki wataendelea kuwepo. Si ajabu kukuta mvuvi au muwindaji kutokuwa na akiba yoyote ya kumtosha kwa siku kadhaa, si bahari, mto au ziwa lipo bhana?sasa kwanini ahangaike, hamna sababu (kwa mawazo yake). Tatizo ni pale ambapo atakosa uwezo wa kuvua ama kwa uzee au ugonjwa, lazima familia itatereka kwa kukosa mahitaji muhimu. Pia kuna kipindi serikali hufunga mito, mabwawa na maziwa ili kuruhusu samaki kuzaliana. Wakati huo huo aliefuga samaki anaweza kuendelea kuishi.
Maisha ya muwindaji na mvuvi ni ya kula na kutumia kile chochote anachokipata, hakuna akiba na wala hakuna kesho. Mfugaji yeye ana akiba ya mifugo yake na huitumia pale ambapo anapata tatizo. Muwindaji hawezi kwenda porini kuchukua wanyama walio hai ili kuwatunza, hana muda wala uvumilivu huo. Muwindaji na mvuvi hawaweki akiba ya walichokipata ama kukiendeleza ili kiwe kikubwa ili kesho kiwasaidie, hawafikiri katika kuzalisha bali kutumia tu. Hawa watu wanakula kila kitu na kusahau kukuza ili kesho kiwape faida. Wanasahau kuwa akiba haiozi.


Mpendwa msomaji mfano wa mfugaji na mvuvi ni mfano uliopo katika jamii zetu.Inawezekana kabisa wewe una tabia zote za mfugaji au una tabia zote za mvuvi/mwindaji. Ni muda sasa wa kujifanyia tathmini. Kuna wale ambao huweka akiba na kukuza vipato vyao ili viwasaidie baadae na hao ndio mfano wa mfugaji na kuna wale ambao hutafuna kila kitu walichojaaliwa kukipata,hawa ndio wavuvi. Bila shaka wewe unajijua upo kundi gani, kundi la mfugaji au kundi la mvuvi. Ni mara nyingi sana unakuta mtu anapata kipato na kuamua kutumia chote hasa mshahara akijua kwamba mwisho wa mwezi ataupata mwingine,huyu hana tofauti na mvuvi mwenye imani na bahari bila kujali kwamba kuna mawimbi, bila kujali kwamba kuna kukauka kwa mito na kupungua kwa kina cha maziwa na samaki kuzaliana. Watu hawa mwisho wa mwezi unaweza kuwakuta wakiwa hawana kitu na kuanza kuishi kwa kukopa. Yeye akipata hela hutumia katika kununua vitu ambavyo haviwezi kumzalishia mali. Mtu huyu ambae ni mvuvi hatakuwa na uwezo wa kusonga mbele hata siku moja. Ataanzaje kwa mfano wakati hana mnyama ambae kesho atazaa na kuwa nao wawili au watatu? Kama unataka kusonga mbele na kufanikisha malengo yako ni muhimu uache kuwa mvuvi na kuamua kufuga, ni muhimu kuana kujiwekea akiba. Kuna msemo wa kiingereza usemao ‘’A dollar saved is a dollar earned’’ ukiwa na maana kwamba ‘’Dola moja iliyowekwa akiba ni dola iliyokwishwa kupatikana’’. 

Katika kitabu kitakatifu cha biblia, kuna mfano wa pacha wawili, mkubwa akiitwa Essau na mdogo akiitwa Yakobo. Essau alikuwa ni mwindaji na Yakobo alikuwa mfugaji. Siku ambayo baba yao alitaka kumbariki Essau alimtuma akawinde amletee nyama aweze kumbariki. Mdogo mtu na mamaye waliamua kumchukua mnyama ambae anafugwa na kumuandaa kisha kumpelekea baba yao Isaka. Mpaka muda huo Essau alikuwa ameshachelewa na hivyo kukosa baraka kutoka kwa baba yake. Laiti kama Esau angelikuwa na wanyama pale nyumbani pengine asingechelewa kupata baraka alizopanga kutoa baba yake kwake. Akiba aliyokuwa nayo Yakobo ilimfanya awahi fursa ya baraka. Ni mara ngapi umezikosa fursa muhimu kwa sababu ya kutokuwa na akiba? Unapokula kumbuka kuna kesho pia.
SOMA: Je mtaji ni kikwazo kwako katika kuanza biashara au kuwekeza?

 Kama utaamua kujiwekea akiba mathalani ya pesa ni muhimu sana kuifanya iendelee  kukua kwa kuizungusha ili iweze kuzalisha nyingine. Mwadishi mmoja aliwahi kusumea kwamba hela isiyozungushwa ni sawa na gazeti la zamani. Gazeti la leo halitakuwa na thamani kesho ama kesho kutwa,matumizi yake ni leo tu. Huwezi kwenda kwa muuza magazeti kununua gazeti la mwezi uliopita, kwanza ni vigumu kulipata. Akiba utakayoipata iwekeze ili kipato chako kizidi kukua. Kila mara jiulize kama wewe ni mfugaji au mvuvi. Acha kununua vitu ambavyo havikuzalishii chochote na uanze kununua vitu vitakavyoongeza kipato chako. Watu ambao tayari ni matajiri na wale wenye akili na mawazo ya kitajiri hawanunui vitu vya anasa kwa kipato au mtaji wao bali kwa faida waipatayo kupitia vyanzo walivyovianzisha. Kwanini umchinje ng’ombe mmoja ulienae kwaajili ya sherehe badala ya kusubiri umchinje ndama wake? Kwa nini ufurahie kwa muda muda mfupi na kuteseka kwa muda wote uliobakia? Kubali kuahirisha mambo yenye kusubiri kwa mambo yasiyoweza kusubiri.

Pia katika mfano wa mfugaji na mvuvi tunona tabia nyingine ya mvuvi ni kutokuwa na subira wala uvumilivu, yeye anachojali ni kutuliza njaa yake ya leo. Wakati mfugaji anavumilia dhoruba zitokanazo na mifugo yake. Anajua kuna magonjwa, njaa nk. Maana yake tunahitaji uvumilivu ili kuweza kukua, huwezi kuzaliwa leo na kutembea kesho. Lazima usubiri. Usione kwamba unapitwa, simamia katika malengo yako na usubiri huku ukiendelea kuboresha mbinu zako za kongeza kipato. Usiogope kuanza na kitu kidogo na kukua kuliko kusubiri mpaka kiwe kikubwa ndipo uanze, ukweli ni kwamba hiyo siku haitakaa ifike. Mfugaji anaweza kuanza na kuku au ng’ombe wawili na baada ya muda fulani akawa nao wengi wakati huo mwingine akisubri apate pesa za kuanza na mia. 

Nakushauri uwe na tabia za mfugaji kuweka akiba kisha kuwekeza katika vitu vyenye kuzalisha. Haiwezekani una vutu vyenye thamani kubwa ndani halafu huna uhakika wa kuishi ikitokea umefukuzwa au kusimamishwa kazi. Maisha ya ajira hayatabiriki hivyo anza kujiwekea akiba na kutafuta kitu cha kufanya. Vitu vyote vizuri utavinunua kwa faida na sio kwa mtaji. Matajiri unawaona walijinyima vitu vya thamani au anasa kwanza ili waweze kutengeneza mifereji ya utajiri.

Nina imani kuwa umenufaika na makala hii. Wasambazie wale uwapendao.

Pia usisahau kupenda ukurasa wetu wa facebook kwa kubonyeza hapa na kujiunga na orodha yetu ya email kwa makala nzuri kila mara. Kwa makala za Afya na Lishe bonyeza hapa

Nickson Yohanes
nmyohanes@gmail.com


Hii ndiyo siri ya kuweza kupokea au kupata kitu chochote

Habari za leo ndugu msomaji wa mtandao huu wa PAMBAZUKA DAIMA ni matumaini yangu kwamba bado unaendelea kulisukuma gurudumu la maendeleo kwa kufanya kitu bora zaidi ya ulivyofanya jana.

Ndugu msomaji kuna siri katika kila kitu ambacho ukifanikiwa kuijua basi utaweza kufanikiwa katika eneo husika. Kuna siri za kufaulu mitihani shuleni, kuna siri za kuwa na familia bora na kadhalika. Naita siri lakini kiukweli sio siri kwani ni vitu ambavyo tunavijua ama tunaona kwamba havina maana katika maisha yetu na hivyo kutotilia maanani.

Labda nianze kwa kukuuliza swali hili; Ikiwa una ndoo ya maji iliyojaa maji tayari, ukitaka kuweka kitu kingine katika ile ndoo au maji mengine utafanyaje? Majibu yanaweza kuwa mengi lakini jibu la muhimu ni kuyatoa yale maji kwa kumwaga ama kumpa anaehitaji ili upate nafasi ya kuweka kitu kingine. Lakini litakuwa sio jambo jema kumwaga maji wakati kuna anaehitaji. Kwa hiyo basi siri ya kupokea kitu chochote ni kutoa, ndio kutoa kwa anaehitaji ili nawe upate nafasi ya kupokea kitu kipya. Kama hutatoa na wewe umeshajaza vitu katika sehemu yako ni dhahiri kwamba hakutakuwa na nafasi ya kupokea kitu kipya. Ndio maana tunashauriwa kutoa ili nasi tupokee, huwezi kuwa mtu wa kupokea pekee.


Tunapozungumza suala la utoaji tunamaanisha kitu chochote ambacho kinaweza kuwa msaada kwa mtu mwingine. Suala la kutoa sio lazima uombwe, ni muhimu zaidi kama ukitoa bila msukumo kutoka nje. Kitabu cha biblia kinawaasa watu kuwa kutoa ni bora kuliko kupokea na pia utapokea kadiri nawe unavyotoa, tena maradufu. Unapozungumzia suala la kutoa watu wengi hupeleka akili zao katika pesa. Kutoa pesa ni muhimu pia, lakini je kama huna pesa huna sifa ya kutoa? Unaweza kutoa kitu chochote kwa mtu yeyote ilimradi kina msaada kwake. Unaweza kutoa msaada, kutoa elimu, kusaidia wasiojiweza, kufundisha wenzako, kutoa muda wako kwa kusaidia wengine ama kuwatembelea wagonjwa, yatima na wale wanaohitaji faraja na hata kutoa sehemu ya mali zako kwa wengine. Kuna siri kubwa katika utoaji, ni siri ambayo haiwezi kuelezeka kirahisi ni siri kubwa sana ya kupokea chochote. Ila muhimu sana ni kwamba unapotoa kitu usitoe ukingoja shukrani au ukitegemea malipo kwani malipo yake utapata katika muda usioutegemea tena kwa mtu usiyemtegemea. Kuna msemo wa Kiswahili usemao ‘’Tenda wema nenda zako, usingoje shukurani’’.
Soma: Je umepanda nini shambani kwako?

Ndugu yangu unaesoma hapa nawe una kitu cha kutoa kwa watu wengine, usiwe mtu wa kupokea pekee bila kutoa. Kutoa hakukufanyi kufilisika bali kuendelea kuneemeka. Kama kutoa kungekuwa kunafilisi basi bilionea tajiri namba moja duniani Bill Gates angeshafilisika kitambo kwa misaada  anayotoa duniani kupitia mfuko wake wa Bill and Melinda Gates unaohusika kutoa misaada kwa watu masikini kote duniani. Kwa hapa nyumbani Tanzania basi mzee Reginald Mengi angekuwa ameshafilisika kitambo pia maana toka nilivyoanza kumsikia anatoa misaada kwa kweli angekuwa ameshaishiwa. Bilionea namba tatu kwa sasa ambae pia alishakuwa namba moja na mbili katika kipindi cha nyuma Warren Buffet nae ni mtoaji mzuri na amedhamiria kutoa 99%  ya utajiri wake kama misaada katika maisha yake yote. Hii ni tofauti kabisa na dhana hasi iliyojengekwa kwamba watu matajiri ni wabinafsi na wachoyo, jambo ambalo si kweli. Matajiri hupenda kusaidia hasa wale wanaonyesha nia ya kufanya jambo fulani zuri.

Kama wewe ni mwanafunzi na unalijua vizuri somo fulani kuliko mtu mwingine yeyote darasani kwako ukiamua kulifundisha hilo somo kwa wengine, si tu kwamba utakuwa umewasaidia wengine kufaulu somo linalowapa shida bali pia nawe utaimarika katika hilo somo kwa kupokea changamoto na kupokea elimu mpya kutoka kwa wengine.Pia itakusaidia kukumbuka kirahisi na kuonekana bingwa wa somo husika. Utafungua mlango wa wenzako kukusaidia katika masomo mengine ambayo wanayaweza vizuri kuliko wewe. Kinyume chake ni kwamba hutaona mafanikio mazuri katika masomo yako kama utakuwa mbinafsi. Kila mtu anaweza kutoa kitu, hata kama ni kidogo kiasi gani. Ndio maana hata katika dini zetu tunasisitiziwa kutoa zaka katika nyumba za ibada kama shukurani kwa Mungu wetu kwa aliyotujalia kupata.

Inaweza kukuwia vigumu pale unapoanza lakin utaweza kuzoea tabia hiyo ya utoaji kadiri unavyotoa kila mara. Unaweza kuanza kidogo kidogo mpaka pale utakapoona kwamba sasa huoni ugumu katika kutoa. Labda nikupe hadithi ya kweli; Mwaka fulani nikiwa sekondari, tulitoka shule mchana kama ilivyo ada. Tukitembea watatu njiani kuelekea nyumbani mmoja wetu (si mimi) alitoa kiasi fulani cha pesa kwa mlemavu aliekuwa anaomba barabarani, hatua kama tano mbele aliokota mara tano ya pesa aliyotoa kwa yule mlemavu. Unaona katika mfano huu jinsi kutoa kunavyofungua milango mingine, milango ya kupokea. Sikuambii kwamba ukitoa nawe utaokota hela kama rafiki yagu,hapana. Toa kwa kuwa umeguswa na ukiamini kwamba unawasaidia wengine kwa kile ambacho umejaaliwa kuwa nacho. Tahadhari tu kwa upande wa fedha uweze kutofautisha kati ya kutoa kusaidia na kutapanya pesa zako ovyo. Unaweza kuanza kwa kutenga asilimia ya mapato yako kwa kusaidia wengine. Muda wako nao ni wa thamani sana hivyo ni muhimu kuulinda na kutoutoa kwa wale wasiostahili.

Usisahau kupenda ukurasa wetu wa facebook kwa kubonyeza Pambazuka Daima Blog na pia kujiunga na orodha yetu ya barua pepe kupata makala kila mara zitokapo.

Nickson Yohanes
nmyohanes@gmail.com